TFF Yaufungulia Rasmi Uwanja wa KMC: Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza rasmi kuufungulia matumizi Uwanja wa KMC uliopo Dar es Salaam, baada ya kuridhishwa na marekebisho yaliyofanywa kufuatia changamoto za awali za miundombinu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF, uwanja huo ulikuwa umefungiwa matumizi ya mechi za Ligi baada ya kubainika kutokidhi baadhi ya vigezo vya kikanuni vinavyohusu miundombinu ya viwanja.
Makala nyingine: RATIBA YA NBC PREMIER LEAGUE( LIGI KUU TANZANIA BARA) 2025/2026: MECHI ZOTE MUHIMU KUANZIA JANUARI HADI MACHI 15, 2026
Hata hivyo, baada ya maboresho kufanyika, TFF imejiridhisha kuwa masharti yaliyowekwa yamekidhiwa, hivyo kuuruhusu uwanja huo kutumika tena kwa mechi za Ligi.
TFF imeeleza kuwa uamuzi huo umetokana na tathmini ya miundombinu iliyofanywa baada ya marekebisho, hatua inayolenga kuhakikisha viwanja vinavyotumika vinaendana na viwango vinavyokubalika katika uendeshaji wa Ligi.
Pamoja na hatua hiyo, TFF imeendelea kuzikumbusha klabu zote nchini kuwekeza katika kuboresha viwanja vyao vya nyumbani, ikisisitiza kuwa miundombinu bora ni msingi wa kuongeza ushindani, kuvutia mashabiki na kuinua thamani ya Ligi ya Tanzania.
Shirikisho limesisitiza kuwa litaendelea kusimamia kanuni na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya viwanja, ili kuhakikisha mashindano yanafanyika katika mazingira salama na yenye ubora unaostahili.
Taarifa hiyo imetolewa Dar es Salaam na kusainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo, Februari 4, 2026.